Friday, 1 September 2017

Je dhamana ni haki ya kila mtu au ni upendeleo kwa watu fulani fulani? Fahamu maana, aina na vigezo vya kupata thamana



 Je dhamana ni haki ya kila mtu au ni upendeleo kwa watu fulani fulani? Fahamu maana, aina na vigezo vya kupata thamana



Bila shaka utakuwa umewahi kusikia kuhusu neno hili dhamana, inaweza kuwa eidha ni ndugu au rafiki yako alitakiwa kuwekewa dhamana au penginr umewahi kusikia katika vyombo vya habari kuwa fulani na fulani wamepewa au kukataliwa dhamana. 

Katika makala hii nitajikita zaidi katika kutizama nini maana ya dhamana, aina ya dhamana na vigezo vya mtu kupata dhamana. Watu wengi wanakasirika wanaposikia fulani kashitakiwa na baadae wanamuona yupo uraiani bila kujua ni haki ya mtu huyo kikatiba na kisheria bila kujali kuwa kashikiliwa na polisi au kesi ipo katika mahakama.

Wengine huenda mbali zaidi na kudhani Polisi au Hakimu wamepewa rushwa ili kumuachia huru mshukiwa au mtuhumiwa.

Hali kadhalika wengine hudhani vyombo vya dola havichukui au kufuata taratibu zinazotakiwa pindi mtu akipelekwa anaposhitakiwa.


Nini maana ya dhamana?


Neno dhamana sio geni masikioni mwa wengi kwani hata tunapokuwa mitaani huku tunajikuta tunalitumia sana. Kwa mfano mtu akitaka kumkopa mwenzie atamwambia nipe dhamana yako yaani kitu mbadala cha kuweka ili nikupe huo mkopo. Lengo kuu hapa ni kitu kile kitumike kama rehani ili endapo mkopaji atashindwa kurudisha mkopo aliochukua kitu kile kichukuliwe kama fidia ya deni. Huo ni mfano mmojawapo kati ya mifano mingi ninayoweza kukupatia ili uweze kupata picha ya nini maana ya dhamana..

Hali kadhalika kisheria maana zinafanana kabisa kwani ni makubaliano ambayo mshukiwa au mtuhumiwa anayaingia na mahakama au Polisi kwa lengo la kumwachilia huru kutoka kituoni au mahabusu.

Makubaliano hayo yanajumuisha kufuata masharti ambayo mshukiwa au mtuhumiwa atapewa na Polisi au mahakama, kutoa kiasi fulani au kuweka rehani kitu fulani na kadhalika. Lengo kuu hapa ni kumfanya mshukiwa au mtuhumiwa kufuata masharti aliyopewa na eidha Polisi au mahakama ikiwa ni kuhakikisha anafika mahakamani kama atakavyokuwa anahitajika. 


Je dhamana ni haki au upendeleo?


Ndiyo ni haki ya mtu na haitolewi kwa upendeleo. Upo ushahidi mpana sana wa kisheria kulithibitisha hili. Maelezo yatakayofuata yataeleza kwa uchache kuhusiana na jambo hili ili kukupa wewe ndugu msomaji maarifa. Yafuatayo ni maeneo makuu matatu (3) yanayoelezea kwamba dhaman ni haki;




Dhamana ni haki ya mtu kikatiba na kisheria pia. Dhana nzima ya mtu kupewa dhamana imetokea kwenye principle inayoitwa presumption of innocence chini ya Ibara ya 13 (6) (b) cha Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 kwamba hakuna atakaye hukumiwa mpaka mahakama ithibitishe, kwani ndio muhimili pekee unaoweza kusema fulani kakosa na anatakiwa kuhukumiwa kifungoni au kadhalika kama Katiba inavyoelekeza.

Vilevile mtu anatakiwa kufurahia uhuru wake binafsi hali kadhalika uhuru wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kama inayoelekeza Katiba katika ibara ile ya 15 (1) na 17 (1).   

 Kwa mantiki hiyo hakuna sababu za kumtia mtu kizuizini mpaka itakavyothibishwa kuwa mtu huyo anayo hatia kisheria isipokuwa kama mahakama itaona inafaa. Umenipata hapo ndugu msomaji wangu?




Pia, katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura namba 20 katika kifungu kile cha 64 (2) kinahitaji Polisi wamwachilie huru mshukiwa kwa dhamana kama atakuwa katimiza vigezo ambavyo tutakuja kuvitizama baadae kwa undani zaidi. Hali kadhalika Mahakama inatakiwa kufanya vivyo hivyo kama kifungu cha 148 cha Sheria hiyo ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinavyohitaji.


3.       Maamuzi mbalimbali ya Mahakama


Ni wachahe wanaofahamu kwamba maamuzi ya mahakama yanaweza kuwa sheria. Kivipi? Vipo vigezo ambavyo vikitimizwa kwenye kutoa maamuzi yataweza kutumika baadae kama sheria na kumbana Jaji au Hakimu kuamua vinginevyo kwenye kesi zitakazofuatia zinazofanana.

Kwenye kesi ya Tito Douglas Lyimo v Republic 1978 L.T.R n.55 iliamuliwa hivi, kwa ufupi inaweza kuelezwa kwamba mara nyingi kama sio zote dhamana ni haki na sio upendeleo kwa mtuhumiwa isipokuwa makahama imeshawishiwa vinginevyo kwa ushahidi mzito uliotolewa na upande wa mashtaka unapopinga maombi ya dhamana kutolewa. Kutokufanya hivyo kunaweza kupelekea HAKI kupotea.


Aina za dhamana


Zipo aina mbili (2) za dhamana, ambazo ni dhamana ya polisi na ile ya mahakamani. Kama nilivyo kwisha kueleza hapo awali zote hizi ni dhamana na zinatolewa kwa mujibu wa sheria. Kwa sababu nitazichambua katika Makala itakayofuatia kwa undani zaidi hapa nitazielezea aina hizo mbili kwa ufupi ili uweze kupata japo picha ndugu msomaji bila kuchoshwa.


1.       Dhamana inayotolewa Polisi  


Kwa Lugha ya kitaaluma inaitwa ‘Police Bail’. Hii kwa kawaida huwa anapewa mshukiwa ambaye bado yupo chini ya ulinzi wa polisi na hajafikishwa mbele ya mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka. Hapa mtuhumiwa anakuwa amewekwa chini ya ulinzi wa Polisi kwa wakati fulani.

Hali kadhalika Polisi hawaruhusiwi kumweka mtu kizuizini kwa kipindi kisichozidi masaa ishirini na manne isipokuwa kama zipo sababu za msingi kufanya hivyo. Hivyo basi Polisi wana uchaguzi wa eidha kumpeleka huyo mshukiwa mahakamani akasomewe mashtaka au kumwachia kwa kumpa dhamana.


2.       Damana inayotolewa na mahakama 


Hapa zipo pia aina mbili za dhamana zinazoweza kutolewa na mahakama kama vile:  

  •  Dhamana inayotolewa mtuhumiwa anapokuwa anaubiria uamuzi wa shauri lake mahakamani. Hii ni ‘Bail pending trial’ kwa maana ya kwamba inatolewa na mahakama baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa. Hii hutolewa wakati shauri limeshafika mahakamani na mtuhumiwa kashasomewa mashtaka na akapinga shtaka hilo au mashtaka hayo aliyosomewa. Na itakapotokea shtaka hilo au mashtaka hayo yapo katika yale yanayopewa dhamana na amekidhi vile vigezo vinavyotakiwa basi kama akiomba dhmana atapewa dhamana hiyo kwa masharti ambayo mahakama itaona yanafaa.
  • Dhamana anayopewa mtu anapokuwa anasubiria uamuzi wa mahakama dhidi ya rufaa.  Hii inatolewa pale mtu anapotiwa hatiani lakini haridhii uamuzi uliotolewa na mahakama. Hapa hukumu ya adhabu inakuwa imeshatolewa lakini mtuhumiwa haafiki uamuzi wa mahakama na anataka kukata rufaa. Kwa hiyo basi unaiomba mahakama ikupe dhamana uwe huru wakati rufaa yako ikisubiri kutolewa uamuzi. Sio rahisi kupata dhamana ya namna hii kwani mahakama inatizama vitu kadha wa kadha kwani hatari ya mtu kukimbia au kutoroka ni kubwa kwa sababu mtu anakuwa tayari anafahamu ni adhabu ya aina gani ambayo ameadhibiwa.  



Muhimu


Wakati mwingine nitatoa Makala itakayochambua kwa undani aina hizi mbili za dhamana, namna gani zinaombwa, vigezo gani vinavyotumika kupata au kukataliwa kupewa dhamana, faida na hasara za kumdhamini mtu. Nakusihi sana ndugu msomaji usichoke kutembelea ukurasa huu, ku-share kwenye mitandao ya kijamii pamoja na ku-subscibe ili uendelee kujifunza na kupata maarifa zaidi kuhusu sheria kwa ujumla wake. Yupo mtu mmoja amewahi kusema ‘learning is a process’ kwa maana ya kwamba kujifunza ni mchakato.
  

No comments:

Post a Comment