Dhamana inayotolewa
na Mahakama

Kama nilivyowahi kuzungumza katika makala iliyopita inayohusiana na dhamana nilitaja aina mbili za dhamana ambazo ni dhamana inayotolewa mahakamani mtu akiwa anasubiria shauri au rufaa aliyoiwasilisha kusikilizwa na kutolewa uamuzi na mahakama lakini pia niliangazia ile dhamana inayotolewa na polisi pindi mtu anapofikishwa kituo cha Polisi kama mshukiwa.
Nilidokeza pia dhamana huwa
inatolewa na mahakama baada tu ya mtuhumiwa kuomba. Hii hutolewa endapo
mtuhumiwa hakukiri kosa analotuhumiwa. Dhamana hutolewa endapo mwombaji dhamana
katimiza vigezo au masharti ya mahakama.
Mfano wa vigezo au masharti hayo
yanaweza yakawa ni fedha kiasi fulani au hati ya umiliki wa nyumba, awe na
mdhamini au wadhamini, kutia saini katika makubaliano ya kwamba atatimiza
masharti yaliyowekwa na mahakama.
Kwenye mahakama za Wilaya, Mkoa
au Mahakama Kuu utaratibu wa kutoa dhamana unasimamiwa na Sharia ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai sura ya 20 (The Criminal Procedure Act, Cap 20) kwenye kufungu
kile cha 148 hadi 163
Masharti yanayoambatana na dhamana
Dhamana haitolewi hivi hivi tu,
ni lazima iambatane na masharti kadhaa wa kadha. Yapo masharti yanayowekwa na
sheria lakini pia yapo yale ambayo yanayotolewa kutokana na busara za mahakama:
Masharti ya lazima
- Mtuhumiwa kusalimisha Pasipoti au hati nyingine ya kusafiria Polisi kama anayo.
- Mtuhumiwa kuwekewa kizuizi cha kutokuondoka eneo fulani kama vile mji, kijiji au eneo analoishi.
Masharti yanayotolewa na mahakama
kama itakavyoona inafaa
- Kutoa taarifa polisi kila baada ya muda fulani kama mahakama itakavyoagiza.
- Kumtaka mtuhumiwa kutokutembelea maeneo au majengo yaliyotajwa na mahakama.
- Kuepuka kujihusisha na watu fulani kama mahakama itakavyoeleza.
- Na masharti mengine yoyote juu ya hayo kadiri mahakama itakavyoona inafaa.
Muhimu: Orodha hii sio kamilifu kwani
mahakama ina mamlaka kisheria ya kuweka masharti kadiri itakavyoona inafaa,
linaweza likawa ni moja au zaidi ya yaliyotajwa hapo juu, lengo kuu likiwa ni
kuhakikisha mtuhumiwa atakuwepo mahakamani pindi atakapohitajika.
Mazingira yanayopelekea mtu kutokupewa dhamana
Yapo mazingira kadha wa kadha yanayoweza
kupelekea mtu kutokupewa dhamana. Mazingira hayo yamegawanyika sehemu mbili
yaani yale yaliwekwa na sharia ambapo ni lazima yazingatiwe na yale
yanayoamuliwa kadiri mahakama itakavyoona inafaa.
Mazingira ya Kisheria
- Endapo mtuhumiwa amewahi kupewa dhamana akatoroka au kukiuka masharti yake.
- Kama mtuhumiwa amewahi kuadhibiwa kwa kufungwa kifungo jela kisichopungua kipindi cha miaka mitatu. Hapa sharia ina maanisha kifungo cha adhabu na sio ile ya kuwekwa mahabusu au rumande. Kwani ipo tofauti ya mahabusu anayesubiria uamuzi wa kesi inayomuhusu kufikiwa na mtu anayetumikia kifungo kwa kukutwa na hatia. Kuwekwa mahabusu au rumande sio adhabu na sio tunacholenga hapa.
- Mtu anayetuhumiwa na kosa la mauwaji, uhaini, uporaji wa kutumia silaha, utakatishaji wa fedha, makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, kujihusisha na uuzaji au usafirishaji wa dawa za kulevya na makosa ya ugaidi.
- Endapo busara za mahakama zinaona ni vyema akawekwa mahabusu kwa ajili ya usalama wake. Yapo makosa ambayo mtu akiyafanya itakuwa ni hatari kwa usalama wake endapo atarudi mtaani, kwa mfano mtu aliyeuwa ni wazi kabisa raia watakuwa na hasira naye hivyo busara akakaa rumande kwa ajili ya usalama wake.
Mazingira ya Kimahakama
- Uwezekano wa mtuhumiwa kutenda kosa jingine atakapoachiwa kwa dhamana. Hii inaweza kutokea endapo mtuhumiwa ana historia ya kufanya kosa au makosa kama hayo hapo awa
- Uwezekano wa mtuhumiwa kutoroka endapo atapewa dhamana na mahakama. Kwa mfano kama kosa lina uzito kama vile kukutwa na nyara za serikali au kama mtuhumiwa ni mgeni kutoka nchi nyingine.
- Mahakama itaangalia ni kwa kiasi gani kuachiliwa kwa mtuhumiwa kunaweza kuharibu upelelezi na/au kushawishi mashahidi wa upande wa mashtaka. Ni lazima upande wa mashtaka kama wanapopinga dhamana waeleze sababu za msingi zinazoonyesha ya kwamba mtuhumiwa anaweza kuingilia upepelezi au kushawishi mashahi. Mahakama haitokubali sababu za kufikirika tu ‘there must be satisfactory reasonable or solid grounds and not mere hypothetical assumptions’.
- Ukubwa wa adhabu. Ukubwa wa adhabu itakayoweza kutolewa baada ya mtu kutiwa hatiani pia inaweza kuwa ni sababu ya mtu kutokupewa dhamana. Mfano mtuhumiwa kama akikutwa na hatia itampelekea kifungo cha miaka thelathini jela ni wazi kabisa uwezekano wa mtuhumiwa huyo kutoroka mashitaka yaliyopo mahakamani ni mkubwa kwani itakuwa ni rahisi kwake kutaka aishi huru akiwa ametoroka kuliko kufungwa miaka yote hiyo.
- Umri wa mtuhumiwa. Ni wazi kuwa mtu mzee anapotenda kosa ni ngumu sana kutoroka endapo atapewa dhaman sio kama vile ilivyo kwa kijana.
- Utayari wa wadhamini.
Matokeo ya kuvunja Masharti ya Dhamana
- Kati ya eneo ambalo watu wengi
huwa wanajisahau na kujikuta wakilia ni kufanya masihara wanapopewa dhamana
wakidhani ndio wameshakuwa huru kabisa, la hasha! Masharti ya dhamana ni lazima
yazingatiwe kikamilifu na yafuatayo ni baadhi ya yanayoweza kutokea
itakapotokea masharti yamevunjwa:
- Kama mtuhumiwa ametoroka basi mali iliyowekwa dhamana inaweza kuchukuliwa. Ni raha wakati mtu anapoenda kumdhamini mtu anaweka hati reheni kama dhamana ya kuhakikisha mtuhumiwa anakuja mahakamani ila mtuhumiwa anapotoroka anajikiuta kwenye matatizo kama vile ya nyumba au chochote alichowekea dhamana kikiuzwa.
- Kama mtuhumiwa ametoroka Shauri lilopo mahakamani litaendelea kama kawaida bila ya yeye kuwapo. Matokeo yake ni kwamba akija kukamatwa baadae hatoweza kupinga chochote kilichoamuliwa na kifungo chake kitaanza mara moja baada ya kukamatwa.
- Kama hakutoroka ila kavunja masharti mengine ya dhamana basi asifikirie suala la kupewa dhamana tena kwa mara nyingine kwenye shauri hilo alilowekewa dhamana hapo awali.
- Mtuhumiwa atakamatwa popote alipo na kurudishwa mahabusu.
Je ukikataliwa dhamana ufanyeje?
Unatakiwa ukate rufaa. Kama mtu
hakuridhika na uamuzi wa mahakama wa kumnyima dhamana basi anaweza kukata rufaa kwenye mahakama ya juu
ya ile iliyotoa uamuzi ule, mfano kama dhamana ilitolewa na mahakama ya wilaya au
mkoa basi rufaa yake itakatwa Mahakama Kuu.
Kufahamu zaidi kuhusiana na dhamana fuatilia makala iliyopita kupitia link ifuatayo..https://ijuesheriatz.blogspot.com/2017/09/je-dhamana-ni-haki-ya-kila-mtu-au-ni.html?spref=fb