Sunday, 10 September 2017

Jinsi gani uandike mkataba?



Mkataba ni makubaliano baina ya watu au pande kadhaa yenye nguvu kisheria. Mkataba unaweza kuwa  wa maandishi, mdomo au vitendo. 

Mkataba wa maandishi ni aina ya makubaliano yanayoweza kufikiwa na kuwekwa katika mfumo wa kimaandishi. Katika aina hii ya mkataba ni vyema kabisa mambo ya msingi katika makubaliano yakajumuishwa ndani. Kanuni za kiuandishi ni sharti zizingatiwe ili kuondoa utata unaoweza kujitokeza mbeleni kwenye tafsiri.


Mkataba wa mdomo unaweza kufanywa kwa maneno ya mdomo. Kwa mfano unapokwenda dukani kwa Mangi mtaani kununua bidhaa fulani fulani za rejareja huwa hamuandikishiani bali mnakubaliana kwa njia ya mdomo.

Lakini pia tunapopanda daladala ili kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine hatuandikishani mkataba na makondakta bali huwa makubaliano yanafanyika kwa njia ya mdomo kwamba anakufikisha sehemu fulani kituoni unashuka halafu unamlipa nauli. Hii ni baadhi  ya mifano kadhaa ninayoweza kukupa kuhusiana na aina hii ya mkataba.
  

Mkataba wa vitendo ni mkataba amabao unaoweza kufanywa kwa njia ya matendo. Kwa mfano msambazaji wa mchele wa jumla kama kwa kawaida huwa analeta gunia kadhaa za mchele  na anamwachia muuzaji hafafu muuzaji akimaliza kuuza anamlipa yule msambazaji japokuwa hawakuandikishiana popote makubaliano yale yatakuwa na nguvu kisheria kwani mkataba ule tutauita  mkataba au makubaliano ya vitendo (implied contract).


Ni upi mkataba wenye nguvu kisheria? 


Maelezo ya hapo juu yanaweza yakawa ni makubaliano tu na sio mkataba. Ijulikane ya kwamba mikataba yote ni makubaliano ila sio makubaliano yote ni mikataba isipokuwa yamekidhi vigezo vya kimkataba. Vigezo hivyo  vimewekwa na sharia ya mikataba ya Tanzania kwa jina la The Law of Contract Act, [R.E 2002]. Kwenye kifungu cha 10 cha sharia hiyo kinataja baadhi ya vigezo ambayo ni lazima yawepo kwenye makubaliano fulani ili yaweze kuwa mkataba.

Vigezo hivyo ni kama vile lazima kuwe na makubaliano huru baina ya pande zinazohusika katika mkataba. Na makubaliano hayo hayapaswi kufikiwa kwa kushawishiwa na rushwa, kulazimishwa au nguvu.

Lakini pia wahusika wa mkataba ni sharti wawe na uwezo kisheria wa kuingia mkataba. Uwezo wa kisheria unaohitajika ili mtu aweze kuingia mikataba ni kama vile kutimiza umri wa miaka kumi na minane (18) au zaidi na asiwe na tatizo la akili wakati wanaingia makubaliano hayo kwa kiasi ambacho kitaathiri kuingiwa kwa mkataba.

Mkataba pia usiwe na lengo linalokwenda kinyume cha sharia au sera za nchi. Huwezi kufanya mkataba wa kuuziana bangi au dawa za kulevya au kuua mtu au kuuza mwili kingono ukadhani utakuwa na nguvu kisheria, haitowezekana kamwe kwani lengo lake linakwenda kinyume kabisa na sheria au sera za nchi.

Kigezo kingine ni lazima katika mkataba kuwe na mabadilishano ya kitu kwa kitu yanayoruhusiwa na sharia (a lawful consideration). Kwa mfano unapokwenda kununua nyumba kwa kiasi cha shilingi milioni kumi, tunasema hiyo milioni kumi ni consideration ya thamani ya nyumba. Hivyo ni baadhi ya vigezo vichache vinavyotakiwa ili makubaliano yawe mkataba.

Ndugu msomaji wangu pengine unaweza kujiuliza ni nini basi maana ya makubaliano? Na ni kwanini sio makubaliano yote yanaweza kuwa na nguvu kisheria au kuitwa mkataba? Nitalijibu swali hili kwa mifano.

Tuchukulie unae mtoto anasoma kidato cha nne na ukamuahidi simu aina ya SAMSUNG NOTE 5 endapo ataweza kufaulu mitihani yake ya kidato cha nne, ni wazi kabisa haya ni makubaliano tu kati ya mzazi na mwanawe na mtoto hatoweza kwenda kufungua shauri mahakamani kumshtaki mzazi wake kwa sababu hayajaweza kukidhi baadhi ya vigezo vinavyotakiwa na sheria ili yaweze kuwa mkataba. 

Mfano wa pili ni mume anaweza akamuahidi mkewe kumnunulia gari katika sherehe ya kukumbuka siku yake ya kuzaliwa, haya pia ni makubaliano yasiyoweza kufikia uwezo wa kuitwa mkataba kwani mume akishindwa kutimiza alichokiahidi mkewe hawezi kumshtaki mumewe kwa kuvunja mkataba kwani huo haujatimiza vigezo vya kuitwa mkataba.


Jinsi ya kuandaa mkataba wa biashara


Haya ni baadhi ya mambo yanayopaswa yawepo wakati unaandika mkataba wa biashara. Nomba ijulikane kwamba hakuna namna maalumu ya kuandika (draft) mkataba isipokuwa yapo mambo muhimu yanayoyakiwa yawepo katika mkataba:


1. Kichwa cha mkataba.


Huwa kinatangulia mwanzo wa mkataba kabla ya mambo yote. Kichwa cha mkataba kinaweza kuwekwa juu kabisa ya mkataba katikati kama ukipenda. Kichwa cha mkataba kinatakiwa kueleza mkataba huo unahusiana na nini kwa ufupi sana. Kinaposomwa kichwa cha mkataba picha ya mkataba mzima inatakiwa ionekane bila hata ya kuusoma ndani. Mfano inaweza ikawa hivi MKATABA WA MAUZIANO YA NYUMBA


2. Taja majina ya wahusika wa mkataba 


Baada ya kichwa cha mkataba unaweza ukaandika majina ya pande zinazohusika katika mkataba. Kumbuka sio kila mtu anatakiwa kuingia kwenye mkataba kama nilivyokwisha kudokeza. Kwa mfano, muunganiko wa kichwa cha mkataba na majina ya pande husika zinaweza kuwa katika muonekano ufuatao:


MKATABA WA MAUZIANO YA SHAMBA

kati ya

COMFORT M. NGOWI (wa S.L.P 54 Marangu, ambapo kwenye mkataba huu atajulikana kama ‘Muuzaji’)

na

FAITH M. NGOWI (wa S.L.P 432 Mabibo, ambapo katika mkataba huu atajulikana kama ‘Mnunuaji’)


3. Tarehe na mahali mliposainishana mkataba


Hii pia ni shehemu muhimu sana. Ni vyema tarehe ya siku mnayosainishiana mkataba ikawepo bila kusahau mahali. Inaweza ikawa ni mji au wilaya. Mfano: Mkataba huu umefungwa hapa DAR ES SALAAM leo Tarehe 21.08.2017.


4. Siku ya mkataba utakapoanza na kufikia ukomo rasmi


Kama mkataba unategemewa kuanza siku tofauti na ile ambayo wahusika wamesainishiana basi ni sharti kuwepo kifungu kinachoonyesha hivyo. Hii inatokea pale wahusika wa mkataba hawataweza kuonana siku za usoni hivyo mnaweza kusainishana mkataba tarehe fulani halafu mnaweka na kifungu kinachoonyesha siku utakapoanza rasmi. 

Kwa kuongezea tu kama mkataba una siku ya kufikia ukomo ni vyema tarehe ikaandikwa japokuwa hii sio muhimu sana kwani zipo njia nyingine zinazoweza kuufikisha mkataba kwenye ukomo.


5. Kiwango cha fedha kinachotumika 


Kiwango cha fedha kinachotumika katika biashara ni lazima kitajwe. Kwa mfano: Unaweza kuandika hivi ‘Kwamba muuzaji kamuuzia mnunuaji nyumba iliyoko Mabibo yenye namba Mabibo- Mwananchi plot b/480 Ubungo kwa kiasi cha Shilingi za KItanzania Milioni 800.


6. Kitu kinachohusika katika biashara


Ni lazima mkataba utaje ni kitu gani kinachohusika katika biashara mnayoiingia mkataba. Ni vyema ukaweka taarifa zote ambazo unadhani ni muhimu zinazohusiana na kitu hicho.

Rejea kwenye mfano nilioutoa hapo juu ‘Nyumba’ ndio kitu kinachohusika katika biashara. Na kama ambavyo tulivyoweza kuona taarifa kuhusiana na nyumba hiyo zimetolewa kama vile namba ya kiwanja pamoja na sehemu kilipo. Hii itasaidia kuondoa utata pindi litakapotokea tatizo baadae.


7. Namna malipo yatakavyofanyika


Je unataka njia gani itumike katika kufanya malipo? Je ni kwa njia ya Benki au Mkono au M-Pesa au Tigopesa? Je unataka malipo yafanyikeje, yote kwa pamoja au kidogo kidogo? Je unataka ulipwe kwa kutumia pesa ya kitanzania au kigeni? Yote haya unaweza ukayaweka kwenye mkataba kama sehemu ya makubaliano yenu.


8. Sehemu ambayo mngependa mgogoro ushughulikiwe endapo utatokea


Hapa mnaandika ni wapi mngependa mgogoro ushughulikiwe pindi utakapotokea. Je mtapenda kupeleka mgogoro wenu mahakamani au kwenye mabaraza ya usuluhishi? Kama mmoja wenu ni raia wa kigeni je mngependa iwe nchi gani yenye mamlaka ya kushughulikia mgogoro wenu? Kumbuka kama mmekubaliana katika mkataba mgogoro utakapotokea upelekwe sehemu fulani hamna atakayeweza kufanya vinginevyo nje ya makubaliano yanu. 


9. Sheria ambayo mngependa itumike kusimamia mkataba wenu


Maelezo ya hapa yanakaribia kufanana na hayo hapo juu kwenye kipengele namba nane (8). Ni uamuzi wenu kuchagua mnataka sheria ipi itumike kusimamia mkataba wenu. Hii itakuwa ina nafasi sana kama mnaingia mkataba unaohusisha raia wa nchi zaidi ya moja.

10.   Mambo yatakayopelekea mkataba kuvunjika

Mnaweza mkaweka kifungu ambacho kinabeba mambo ambayo kama yakifanyika yatapelekea mkataba wenu kuvunjika. Ni vyema kila upande kwenye makataba ukaguswa kwa namna yake na mambo hayo. Kwa mfano, mnaweza kukubaliana ya kwamba mnunuzi kama akichelewa kufanya malipo kwa muuzaji kwa kipindi cha siku thelathini (30) basi atakuwa amevunja masharti mkataba automatic. 


11. Taarifa


Mnaweza pia mkaweka kifungu ndani ya mkataba ambacho kinatoa anuani ya kutumia taarifa na endapo kama ikitokea kuna taarifa yoyote ambayo inatakiwa kumfikia yeyote anayehusika na mkataba. Mnaweza mkaweka anuani ya sanduku la barua au barua pepe au namba ya simu kama mtakavyokubaliana kwa kila upande. 


12. Mkataba unatakiwa usainiwe na wahusika katika mkataba


Kusaini mkataba ni ishara ya kwamba wahusika wote katika mkataba wamekubali kufungwa na yaliyomo ndani ya mkataba. Kabla hujasaini mkataba wowote sana sana ile inayoandaliwa na upande mmoja ‘standard form contract’ mfano wa ile tunayoiombea mikopo Benki uisome kwanza kwani kusaini mkataba kuna maana kubwa sana kuwa umekubali kubanwa na masharti yaliyomo ndani kama nilivyokwisha kuelezea, huwezi kusema baadae jamani sikusoma! utabanwa hata kama hukuusoma.


13. Mashahidi nao wanatakiwa kusaini


Hawa ni vizuri wasipungue wawili yaani mmoja kutoka kila upande. Hawa kazi yao ni kuthibitisha ya kwamba mkataba huu umesainiwa na wahusika mbele yao. Mashahidi wanatakiwa wawe ni watu wenye vigezo vya kuwa mashahidi yaani wasiwe watoto au watu wenye upungufu wa akili wakati wa kusaini mkataba.


Angalizo: Hivyo nilivyoviaja hapo juu ni mfano wa mambo yale muhimu yanayotakiwa katika mkataba, hivyo basi pande husika katika mkataba mnaweza kukubaliana mnavyotaka isipokuwa vipengele vyenu visiende kinyume na sheria za nchi. Pia ijulikane ya kwamba mikataba inatofautiana. Ni wazi mkataba wa kuuziana gari hauwezi kufanana na ule ya kuuza au kukodisha nyumba. Kwa maana hiyo nilichokifanya hapa ndugu msomaji wangu ni kukupa mwanga namna mkataba unatakiwa kuandikwa vingine utajiongeza.